‘Hadithi ya kale, inayoishi’
HUSSEIN O. MOLITO
0718 97 56 59/ 0765 68 4870
“binti yangu, umeipata wapi roho ya kikatili kama hiyo?” Mohammed aliuliza na kumfanya Rabia aone aibu na kutazama chini.
Mwendo wa kuifuata barabara ukfikia kwenye kona, na baadae kwenye mzunguko na kuwajulisha kuwa wameshafika kwenye geti la kuingilia hospitali ya Muhimbili. Walichukua kadi ndogo kwa mlinzi na kuifuata gari ya polisi hadi sehemu ya wodi ya wagonjwa mahututi. Binti huyo akapokelewa, lilipohitajika jina moja kwa mtu aliye karibu naye, Samira alikubali liandikwe jina lake.
Watu wa huduma ya kwanza waliwahi na kitanda. Haraka akawahishwa wodini katika harakati za kuyapigania maisha yake.
**************
Daktari alitoka akiwa na karatasi mkononi, akaita jina la mgonjwa. Inspekta Salim alienda kwa daktari akiongozana na Salehe.
“majibu ya X - Ray yanasema hajavunjika popote. Hivyo nimeandika hapa dawa za kutuliza maumivu. Utapita hapo dirishani na kuchukua.”
Yalikua majibu mazuri yaliyotoa tabasamu kwa wote wawili. Walipita dirishani na kuchukua dawa. Baada ya hapo Inspekta Salim akaenda kwenye mgahawa mmoja na kuchukua chakula.
Akampeleka Salehe nyumbani kwake, baada ya kuhakikisha amejikomea mlango, akawasha gari hadi nyumbani kwa mpenzi wake.
“pole na mitihani mume wangu.” alipokelewa kwa sauti laini iliyomuondoa uchovu aliokua nao.
“Ahsante, hata hivyo mi sikai...” kabla hajaoendelea, mpenzi wake akabadilika sura na vitendo. Kutoka furaha hadi hali ya kususa.
“Nisikilize kwanza... Mi nilipanga nilale hapa usiku wa leo, ila kuna tukio kubwa limetokea na hivi sasa nahitajika niwe Muhimbili. Usichukie kipenzi, nikiwahi kutoka huko; nakuja huku moja kwa moja.” Inspekta Salim akabembeleza huku akiwa amemkumbatia mpenzi wake kwa nyuma.
“Naomba nikuambie kitu, kama kweli unataka niendelee kukufurahia.” Zamda aliongea hayo na kumgeukia mpenzi wake wakiwa katika hali ileile ya kukumbatiana.
“sema malaika wangu.” Inspekta akajibu huku akiachia tabasamu.
“hata ukirudi alfajiri, ila upitie hapa kwangu. Ulale mpaka muda wako wa kwenda kazini.” Zamda akaongea hayo huku uso wake ukiwa hauna hata chembe ya tabasamu.
“hilo tu, sema lengine laazizi.”
“na usipokuja?”
“Lazima nije mke wangu, labda yanikute mauti huko nji..” kabla hajamalizia, Shani akamziba mdomo.
“mara ngapi nimekuambia usinitajie maswala ya kifo. Darling nakupenda na sihitaji kukukosa.” Zamda akaongea kwa sauti ya kudeka huku akijilaza kifuani.
“nafahamu kama unanipenda, na dua zako zinaninusuru kila leo. Mimi naamini tutaishi muda mrefu hadi kuwaona vitukuu vyetu.”
Maneno hayo ya faraja yakaleta tabasamu kwa binti mrembo Zamda. Naye Inspekta akaaga kwa mara nyingine na kuruhusiwa kutoka.
Akafunga safari hadi hospitali ya Taifa Muhimbili. Ndipo alipompigia simu Samira ili ampatie maelekezo.
“siye tupo hapa kwenye mabenchi.. Tunasubiria tu maajabu ya Muumba katika kuyapigania maisha ya binti aliyeokoa maisha yangu.” Samira akajibu na kumfanya Inspekta Salim kusogea eneo hilo na kwenda kuegesha gari kwenye maegesho yaliyoruhusiwa.
Alifanikiwa kuonana na Samira akiwa na familia yake.
“Huyu ni baba yangu mzazi, anaitwa Mohammed; huyu ni dada yangu wa kuniachia ziwa... Anaitwa Rabia.” Samira alitambulisha na kumfanya Inspekta Salim ashikane nao mikono kwa mara nyingine.
“Baba, dada... Huyu ni Inspekta Salim. kwa kipindi hiki yupo karibu na mimi kwa haya majanga yote yanayoendelea kunikumba kila leo.” Samira aliongea hayo na kuwafanya watu hao watambuane kwa majina na vyeo vyao.
Yaliwachukua masaa mengine matatu kusubiri hapo, kabla jina la Samira kuitwa. Samira aliongozana na Inspekta Salim. Ila utaratibu wa kuingia mtu mmoja tu humo ndani, ulimfanya Inspekta Salim kutumia cheo chake na kuruhusiwa kuingia.
Waliweza kumuona yule kiumbe akipumulia mashine ya kumpatia hewa safi ya Oxygen. Walimtazama mgongoni ambapo alishafanyiwa upasuaji na muda huo alikua amebandikwa bandeji nyingi zilizoloa damu nyeusi.
Daktari aliwafuata na kuwapa pole.
“hali ya mgonjwa ni mbaya sana. Hata mapigo yake ya moyo hayadundi ipasavyo. Hivyo hapa tunajitahidi tu kuyapambania maisha yake kwa hizo mashine. Lakini hali si shwari.” Daktari aliongea hayo na kuwatazama Inspekta Salim na Samira.
Roho ya kike ikamtafuna Samira kwa kile alichokiona na kusikia kutoka kwa daktari, akajikuta akianza kulia palepale. Inspekta Salim alimtoa nje na kwenda kumkumbatia dada yake.
“vipi, huyo kiumbe amekufa?” Mohammed akauliza.
“hapana, ila hali yake ni mbaya sana. Sidhani kama atachukua hata masaa mawili.” Inspekta Salima akathibitisha hayo na kuwafanya waliopo nje kuingiwa na simanzi.
***********
Akiwa na ghadhabu, alitulia kwenye gari yake kwa muda kabla hajachukua uamuzi wa kuiwasha na kuondoka.
“Dokta Kelvin... Dokta Kelvin.” akaongea kwa sauti iliyojaa hasira huku akijiangalia kwenye kioo kidogo kilichopo mbele yake.
“Sauti ya kifo inaweza kukuita muda wowote.. Muda wowote ule kuanzia sasa.”
Dokta Miley akaongea hayo na kuwasha gari yake, akaitoa eneo hilo kwa kasi.
Akiwa njiani, simu ikaita, jina la Dokta Maliki likatokea kwenye kioo cha simu yake.
“Niambie ndugu yangu.” akaipokea kwa sauti iliyojaa upole, ila moyoni mwake akiwa na fukuto kubwa lililokua linamkereketa. Kutokea kwa Dokta Kelvin wakati akikaribia kutimiza azma yake, kulimfanya achafukwe nafsi yake.
“vipi, umefanikiwa?” Dokta Maliki akauliza swali lililomuongezea machungu, ghadhabu na fadhaa kwa wakati mmoja.
“kuna mshenzi amekuja kuleta taarifa ya msiba katikati ya shughuli..nadhani na yeye kifo chake kinapiga jaramba.” Dokta Miley akaongea huku akiwa makini na usukani. Maana mwendo aliokua akiendesha gari haukua rafiki kwa kufanya jambo lingine tofauti na uendeshaji.
“leo kweli tumefeli mazima.”
Kauli ya kukata tamaa, ndo iliyomfanya Dokta Miley aegeshe gari pembeni. Maana mshtuko wake ulitaka kumsababishia ajali mbaya kwa kugongana na roli lililokua limeomba njia kwa kumuwashia taa za hatari.
“wale washenzi wameshindwa kumuua Samira?” Dokta Miley akafoka.
“hata mimi nimekasirika balaa.. Mbaya zaidi risasi walizofyatua kwa ajili ya kumuua Samira, wamempiga mtu mwengine.”
Taarifa hizo zikawa za kuogepesha zaidi kwa Dokta Miley.
“naomba uniambie kuwa hawajakamatwa na wala hawajaonekana...” Dokta Miley akaongea huku moyo wake ukimdunda kwa hofu.
“hilo ndo la kushukuru.. Maana tulikua tunaukimbia mji sasa hivi. Maovu yote yangebumbuluka na mwisho wa siku tungefungwa miaka milioni 20 gerezani.” Dokta Maliki akaongea hayo na kumfanya Dokta Miley ashushe Pumzi.
“acha nifike kwanza hapo, kisha tutaongea vizuri. Maana naona kama hili dili linataka kututia mawenge.”
“Sawa.” Dakta Maliki akaongea hayo na kukata simu.
Kutokana na barabara kutokua na foleni nyakati hizo, Dokta Miley alitumia dakika ishirini tu kufika kwenye maficho yao.
“bado lisaa limoja tu tukaangalie michanganyiko yetu.” Dokta Maliki aliongea hayo baada ya kuangalia saa yake.
“nadhani italeta majibu mazuri. Hapa nawaza tu vile tutakavyoweza kuwa matajiri wakubwa hapa Afrika.” Dokta Miley akaongea maneno hayo na kumuangalia Dokta Maliki. Naye akaitikia kwa kutikisa kichwa.
Kusubiria dakika hamsini ili kutimia kile walichokihangia kwa muda mrefu, ilikua kama mwaka kwao. Walikaa, walilala, bado muda ulikua kama unasukumwa.
Hatimaye muda ukafika, mtambo maalumu waliotumia kuchanganyia michanganyiko yao ukafunguka.
Ulionekana uji mzito sana wa rangi ya kijani. Wote wawili wakaangaliana kisha wakatabasamu.
“haina haja ya kupoteza muda, tutafute mnyama wa kumjaribia.” Dokta Miley akaongea na kumtazama Dokta Maliki ambaye alionekana kuendelea kuchunguza mchanganyiko huo kwa kutumbukiza kifaa cha kupima joto.
“hatakiwi myama tu, bali mnyama jamii ya binaadamu. Aidha sokwe ama nyani.” Dokta Maliki akatoa kauli hiyo iliyofanya Dokta Miley akune kichwa.
“Sasa tutawapata wapi hao wanyama.... Na isitoshe hii michanganyiko hata hatujui inachukua muda gari kuishiwa nguvu kama haijahifadhiwa.” Dokta Miley akaongea huku akizunguka huku na huko.
“itachukua masaa sabini na mbili. Hivyo kama tukikosa hao wanyama, itabidi tumfanyie binaadamu majaribio.” Dokta Maliki akatoa wazo. Hapo ndipo Dokta Miley alipomuangalia na kuachia tabasamu.
Haya, michanganyiko imefanikiwa, ila wanahitaji majaribio ili kujua huo ugonjwa mpya unaleta madhara gani na watatumia dawa gani kuutibu. Je wataanza kuteka watu na kuanza kuwafanyia majaribio ili lengo lao litimie?
Vipi kuhusu kiumbe wa ajabu, hali yake ni mbaya na daktari amethibitisha kuwa hawezi kupona kutokana na damu zilizomtoka na kuathirika kwa mfumo wake wa upumuaji...
Tukutane tena Kesho iwapo tu nitapata share za kutosha, like kama zote na comment zenye kunionesha kama kweli mmesoma na mmeifurahia.
Muwe na usiku mwema.








0 comments:
Post a Comment
comment