TYPHIN 08
‘Hadithi ya kale, inayoishi’
HUSSEIN O. MOLITO
0718 97 56 59/ 0765 68 4870
“nitadili na Mtafiti Gibson, maana mimi ndo mwangalizi wake kule hospitali. Wewe andaa watu wa kuuondoa uhai wa Samira.” Dokta Miley akagawa majukumu na wote wakakubaliana nayo.
***********
Juhudi za madaktari wazoefu, pamoja na Kundra na Muumba ardhi na vilivyomo,zilionesha ahueni kwa mgonjwa aliyekaribia kupoteza maisha. Upasuaji mkubwa uliofanyika kwa kutoa miba ndani ya mwili pamoja na kuziba majeraha makubwa kwa kushona nyuzi nyingi, ndo yaliyoweza kumfanya mgonjwa huyo kuhamishwa chumba cha wagonjwa mahututi, hadi kwenye chumba maalumu ambacho waliandaliwa manesi wa kuhakikisha wanampatia mgonjwa mahitaji yote muhimu. Maana serikali ilikua inamtegemea sana mtu huyo katika tafiti za maswala ya baharini.
Akiwa chumbani, mgonjwa aliyekaribia kufa akapata ahueni, akafumbua macho. Tukio hilo lilimshtua nesi na kumfanya atoke mbio hadi kwenye chumba cha Daktari.
“Dokta, mgonjwa amefumbua macho.” Nesi akatoa maelezo yaliyofanya dakati huyo atabasamu na kunyanyuka kitini. Akamfuata nesi huyo mguu mosi, mguu pili hadi kwenye chumba cha mgonjwa.
“Sasa yale matumaini tuliyokua tunayasubiria, yameleta majibu mapema.” Daktri akaongea maneno hayo na kuchukua jukumu la kuanza kumpima vipimo mbalimbali.
Daktari aligundua kitu kingine, japokua Mtafiti Gibson alikua amefumbua macho, ila kumbukumbu zake bado hazijarejea.
“anahitaji uangalizi wa karibu sana. Mimi muda wangu wa kuwepo hapa hospitali umeisha. Dokta Miley akifika utampa hii karatasi ya vipimo nilivyompima. Yeye atajua kipi kitafuata baada ya hapa.” Daktari akatoa maelekezo kwa nesi huyo kisha akaondoka.
Nusu saa baadae, dokta Miley akafika hospitali na kwenda moja kwa moja kwenye chumba cha mgonjwa, alishtuka baada ya kumuona amefumbua macho.
“Hana kumbukumbu, Dokta Kelvin ameniachia hii karatasi ya baadhi ya vipimo alivyochukua. Amesema nikupatie.”
Dokta Miley akaichukua karatasi hiyo na kuanza kusoma baadhi ya mambo yaliyoandikwa.
“unaweza kuendelea na shughuli zingine… we niache tu na mgonjwa.” Dokta Miley akatoa kauli hiyo. Nesi bila kufahamu dhamira ya Dokta Miley, akatoka na kuwaacha watu hao wawili tu kwenye chumba hicho.
*************
Baada ya safari ya muda mfupi, Samira aliwasili nyumbani kwake. Bado alikua na hofu kubwa juu ya Watafiti wenzake. Alipitiliza chumbani kwake na kujilaza kitandani. Alianza kuchojoa nguo zake taratibu na kuelekea bafuni. Huko akajitumbukiza kwenye jakuzi. Alimaliza saa nzima huko akitafakari hiki na kile.
Alijitoa kwenye jakuzi taratibu na kwenda kitandani kwake akiwa utupu. Akachukua taulo na kujifuta maji, kisha akajifunga kifuani mwake.
Kila apatapo jambo zito, hupenda kuwasiliana na baba yake. Maana siku hiyo tayari Mzee Mohammed alikua Dar. Alichukua simu yake na kumpiga.
“niambie binti yangu mpendwa.” Mohammed aliongea baada ya salamu.
“baba, Watafiti wenzangu hawajaonekana mpaka leo hii. Hata simu zao hazipatikani. Kingine cha kutia wasiwasi, kuna watu wasiojulikana wamevamia maabara yetu.” Samira akatoa taarifa hizo kwa baba yake.
“Sasa umetoa taarifa polisi?”
“ndio baba, na Inspekta ameshauri tufunge Maabara kwa muda ili kupisha upelelezi, baba naanza kuogopa.” Samira akaongea na kumfanya Baba yake naye apatwe na hofu.
“ni nyema ukaenda kukaa kwa dada yako mpaka hili vuguvugu liishe. Binti yangu unakutana na visanga wiki hii, au kuna mtu umepishana naye kauli?”
“hapana baba, nahisi ni watu wabaya tu ambao hawapendi vile serikali inavyotuamini na kufanya kazi na sisi.” Maelezo ya Samira yakamfanya baba akusanye vitu vyake.
“upo nyumbani muda huu?” akauliza.
“Ndio baba.”
“jiandae, nakuja na Rabia hapo kwako kukuchukua.” Mohammed aliongea hayo na kukata simu.
“funga vitu vyako, mdogo wako yupo hatarini.. fanya hima tumfuate.” Mohammed aliongea maneno hayo na kumfanya Rabia ashangae.
“kakumbwa na balaa gani tena mdogo wangu?” Rabia akauliza huku na yeye akiweka vitu vyake kwenye mkoba.
“ni mambo ya kazini kwao, nadhani yeye mwenyewe atatueleza kinaga ubaga kuhusiana na hili.” akaongea na kumazama mtoto wake ambaye alikua anamalizia kuweka laptop yake kwenye mkoba. Akaongozana na binti yake hadi alipopaki gari yake, safari ya kwenda kwa Samira ikaanza.
Walipofika nyumbani kwa Samira, waliona kuna gari aina ya Noah nyeusi ikitoka eneo hilo. Iliwashangaza kidogo, maana nyumba anayoishi Samira ilikua ni ya mwisho kwenye mtaa huo. Hivyo gari yoyote iliyotoka hapo, ilimaanisha kua ilikua inatoka nyumbani kwa Samira.
“baba nina wasiwasi, huenda si watu wazuri hawa tuliopishana nao. Mbona walipotuona sisi tunakuja wamegeuza gari haraka?” Rabia akiongea maneno yaliyomtia hofu baba yake. Wakati huo walilishalifikia geti la nyumba ya Samira. Baba akachukua simu yake na kumpigia.
“Haloo baba.” Samira akaongea na kumfanya baba yake ashushe pumzi.
“wavaa mawe huko ndani… twende zetu. Muda si rafiki huu.” Mohammed aliongea hayo na kukata simu.
Samira alimalizia hereni zake na kuweka nguo kadhaa kwenye begi lake. Kisha akatoka na kumuachia mlinzi maagizo.
“huyo unayemuachia nyumba si mlinzi , nadhani unahitaji wale wenye bunduki, huyo mwenye kirungu hawezi kukusaidia ukivamiwa. Zaidi atakimbia tu na kukuachia dhahma.” Mohammed akaongea hayo na kuwafanya binti zake wacheke.
Mara zote Mohammed anakua baba bora kwa watoto wake. Huwezi jua kama ni baba na binti zake kwa jinsi walivyoshibana na kuwapa uhuru. Ilifikia hatua hata mama yao kutamani angejumuika nao kwa jinsi wanavyomtumia picha wakiwa sehemu mbalimbali walizopelekwa na baba yao.
Jioni hiyo aliwapeleka mahala tulivu ili wapate chakula cha usiku pamoja, kisha ndo awapeleke wakapumzike na yeye ndo arudi kwake.
Wakati wanafurahia chakula, hawakujua kama walikua wanafuatiliwa. Ile Noah nyeusi waliyopishana nayo awali, haikuwa ya heri kwa binti Mohammed. Kufika kwao ndo ilikua salama ya Samira, maana tayari vijana walishapewa kazi kwa ajili kuondoa uhai wake.
“bosi, tumefanikiwa kuwafuatilia hadi hapa Tripple Seven. hapa tulipo tunayo nafasi ya kumpiga risasi pia, au tuendelee kusubiri hadi atakaporudishwa?.” mmoja wa watu makatili, akatoa taarifa kwa mtu aliyempa kazi.
“sasa unasubiri nini kufanya kazi yako kama nafasi ipo?… muulie mbali.” Sauti ya mamlaka ikasikika upande wa pili, simu ikakatwa.
Taratibu kijana huyo alifungua begi lake na kutoa bunduki yenye uwezo wa kupiga masafa mrefu. Akafunga kiwambo cha sauti ili aweze kufanya tukio lake bila watu wengine kushtushwa na sauti ya risasi pindi atakapoifyatua..
Mimi na wewe hatujui nini kitakachomkumba binti Mohammed, vipi kuhusu uhai wa Mtafiti Gibson? Tukutane tena Jumatatu.
Simulizi hii itakua inaruka Jumatatu, Jumatano, Ijumaa na Jumamosi.








0 comments:
Post a Comment
comment