‘Hadithi ya kale, inayoishi’
HUSSEIN O. MOLITO
0718 97 56 59/ 0765 68 4870
“Nipo hapa kuku sikiliza, niambie ilikuaje..” Inspekta Salim akaongea, safari hii akakunja sura, alimaanisha muda wake wa kuwa kazini umefika.
Samira akameza fundo la mate ili aanze kuelezea mkasa mzima.
Ilikua mishale ya saa kumi na mbili asubuhi. Anga lilikasirika kwa kuonesha ndita zake. Weusi ukaleta ishara ya mvua huku ikihakikishiwa na manyunyu yaliyoanza kushuka kwa kudengua.
Samira akiwa kwenye gari yake ndogo, aliruhusu weypa ziaze kufanya kazi yake ili kioo kisitengeneze ukungu.
Akiwa anafanya mambo mmawili kwa wakati mmoja, yaani kuendesha gari huku akiwa anaongea na mtu kupitia simu yake ya mkononi, alifanikiwa kumuona mtu akiwa kando ya barabara akiwa uchi wa myama. Tena akitembea bila wasi wowote.
Kwakua mtu huyo analingana naye jinsia, hakutaka kumpita bila kumsitiri kwa mavazi. Akasimamisha gari ili apate kumuhoji, ikiwezekana ampatie baibui lake auondakane na udhalilishaji wa jinsia ya kike.
Kwakua alisimamisha gari mita kadhaa, ilimchukua sekude kadhaa kumsubiri mtu huyo aweze kumfikia.
Alimshuhudia binti huyo mdogo akiendelea na safari bila kuonesha kujali idadi ndogo ya watu waliokua wakimshangaa, akashuka na kujaribu kumsalimia.
“Mambo dada.” Samira alipaza sauti ambayo aliamini msichana huyo angemsikia.
Sauti yake kupea bila mtu huyo kuonesha ishara zozote za kujali, ilimpa tafsiri tofauti ubongoni mmwake. Alihisi huoenda binti huyo alikua na matatizo ya masikio. Akamfuata kwa kuongeza mwendo na kulingana naye.
“Mambo, nakusalimia.” Samira akarudia kwa sauti kubwa ili apate kuhakikisha kama binti huyo alikua na matatizo ya masikio kama alivyodhani awali.
Safari hii binti huyo alisimama na kuanza kumshangaa. Alilitazama baibui la Samira na kulinusa. Kwa Samira kikajengeka kitu kingine kwenye fikra zake. Sasa alihisi binti huyo alikua na matatizo ya akili.
“Unahitaji hii nguo?” Samira akauliza baada ya kumuona binti huyo akizidi kulivuta baibui lake. Binti huyo hakujibu, zaidi aliacha kulivuta baibui na kuushika mtandio wa Samira.
Kwakua palishaanza kupambazuka, magari kadhaa yaliyokua yanapita kwenye barabara hiyo, yalishusha vioo na kushuhudia tukio hilo la binti aliyekua utupu wa mavazi.
Samira akavua Baibui lake la gharama na kumvisha binti huyo. Cha ajabu bado alihitaji na mtandio.
“Mimi siwezi kutembea kichwa wazi... Twende nyumbani nikakupe mtandio mwengine, na viatu.” Samira aliongea na kumshika mkono binti huyo ambaye alikubali kumfuata huku akiendelea kuushangaa mtandio wa Samira wenye marembo.
Akamuingiza binti huyo kwenye gari, bado hata humo ndani alionekana kuwa mgeni wa kila kitu. Alishangaa siti za gari na kubonyeza vitu mbalimbali vilivyoweza kufikiwa na mkono wake.
Samira aliingia upande wa dereva na kuwasha gari.
“Vaa mkanda, kama mimi nilivyofanya.” Samira akaongea na kumfanya binti huyo naye avae mkanda vyema kabisa.
“Kumbe anaelewa, kipi kilichomsibu binti huyu mdogo?” Samira alijisemea mwenyewe kwenye moyo wake na kugeuza gari kurudi nyumbani.
Kwakua alihisi atachelewa kufika kazini, aliamua kutoa taarifa kwa mkuu wa kitengo.
“Habari Mr. Gibson.” Samira alisalimia baada ya simu kupokelewa.
“Salama, hofu yangu juu yako.” Sauti ya upande wa pili ikajibu.
“Nimekutana na kisanga huku njiani. Hivyo narudi nyumbani maramoja. Huenda nikachelewa kufika Maabara.” Samira akaongea na kumuangalia abiria wake ambaye alikua akiyashangaa manyoa yaliyokua kwenye dashboard ya gari hiyo.
“Sawa, ila ni muhimu sana kufika, kuna samaki ameoneka juu ya maji, amekufa. Ni wale Dragon fish. Sasa unaweza kuhisi tu ameuliwaje kutokana na kukaa kwake chini ya maji yenye kina kirefu?” Mtafiti akaongea na kumfanya Samira ashtuke baada ya kupewa taarifa hizo ngeni masikioni mwake.
“Kweli inahitajika utafiti wa kina. Nakuahidi kuwahi kufika kadri niwezavyo.” Samira akajibu na kukata simu.
Akaiweka simu yake kwenye eneo la kuwekea vitu mbalimbali vidogo. Binti aliyekua pembani yake akaiwahi simu hiyo na kuiweka sikioni.
“Kweli inahitajika utafiti wa kina. Nakuahidi kuwahi kufika kadri niwezavyo.” Akarudia kauli ya mwisho iliyotamkwa na Samira na kuigiza kukata simu. Kisha akirudisha pale ilipowekwa.
Tukio hilo likazidi kumshangaza Samira. Maana baada ya kufanya hivyo, binti huyo aliendelea kushangaa vitu mbalimbali alivyokua anaviona barabarani.
Baada ya kuliegesha kwenye mfumo wa mtu aliyehitaji kurudi alipotoka, akazima gari.
“Nisubiri hapa, nakuja sasa hivi.” Samira akaongea na kushuka kwenye gari. Hata hivyo binti huyo akakaidi na kushuka.
Samira akashika kichwa na kuongoza ndani, binti huyo akamfuta.
Alikomea sebuleni baada ya kuona vitu vingi vigeni machoni mwake. Alichukua rimonti iliyokua sebuleni na kuibonyeza, Tv ikawaka na kumfana ashtuke sana.
Samira akaamua kumacha mgeni wake sebuleni na yeye akaelekea chumbani. Huko alibadilisha mtandio na kuvaa baibui lengine. Akachukua Suruali, fulana na viatu, kisha akatoka na mtandio sebuleni.
Alishangaa kumuona mgeni wake akiwa amemkamata samaki wa mapambo mkononi.
“Hapana, kama unanjaa nitakukaangia samaki mwengine. Huyo mbichi,mrudishe kwenye maji.” Samira aliongea, ila binti huyo hakumsikiliza. Akamuweka samaki huyo mdomoni na kummeza.
Ilikua ni ajabu sana kutokea, ila Samira alijionea mwenyewe vitimbwi hivyo.
Alipotupa macho yake kwenye Kwelamu la kufugia samaki, hakukua na samaki hata mmoja. Wote walishamezwa wakiwa wazima na binti huyo.
Licha ya ujasiri alionao kwa kufanya tafiti mbalimbali hasa kwenye maji ya kina kirefu, ila alianza kuingiwa na hofu juu ya kiumbe huyo aliyemkaribisha nyumbani kwake.
Aliamua kumpatia nguo avae. Alishangaa alipomuona anavaa juu ya baibui, akamuwahi.
“Sina nguo ya ndani amayo sikuivaa, ningekupatia. Ila kwa sasa anaza kuvaa hii suruali, kisha vaa hili fulana na baibui lije juu yake.” Samira akamuelekeza na kumsaidia vingine ili asimcheleweshe. akamtanda ushungi ule aliutamani wakiwa njiani.
“Twende.” Samira akaongea na binti huyo akachukua rimonti na kuzima tv.
Akaingia naye kwenye gari. Safari hii wala hakumuelekeza kufunga mkanda, alifunga mwenyewe na kutulia.
“Nikupeleke wapi?” Samira akauliza, binti hakujibu kitu chochote.
“Mimi naelekea kazini, hatuwezi kwenda wote huko.” Samira akaendelea kuongea peke yake, hakuna jibu alilpatiwa. Akaamua kuwasha gari na kuondoka eneo hilo.
Baada ya mwendo mrefu. Aliegesha gari yake kwenye kituo kimoja wapo cha daladala na kumuamuru msichana huyo ashuke. Alifungua pochi yake na kumpatia pesa.
Binti huyo hakuzipokea pesa hizo, alifungua mkanda na kutoka.
Samira hakutaka kumlazimisha wala kumfuatilia tena, zaidi ya kuondoa gari eneo hilo na kuondoka.
Alifka Maabara binafsi ya Mtafiti anayeaminiwa na serikali. Alimuona Mr. Gibson akiwa bize akiendelea kumchunguza Samaki huyo aina ya Dragon.
“Afadhali umekuja, hebu angalia hii mikwaruzo mfano wa kucha, unahisi ni samaki gani aliyemdhuru huyu Dragon?” Mtafiti Gibson akamdaka Samira baada tu ya kuwasili.
Samira naye akaingia kazini moja kwa moja na kuanza uchunguzi.
“Ni ajabu sana, bila shaka kwenye ukanda wetu kuna samaki ambaye bado dunia haijamtambua. Yatupasa tumfanyie utafiti ili tuweze kumgundua.” Samira akachangia mada na kumfanya Mtafiti Gibson atabasamu.
Muda huohuo akafika mtumishi wa serikali aliyevalia nguo za kijeshi.
“Mr Faridi, kitambo sana sijakuona.” Mtafiti akamlaki mgeni wake na kumuacha Samira kwenye meza yao ya utafiti. Wakatoka kidogo na kwenda kukaa eneo lenye makochi.
“Ndugu yangu nimekuja kukupa taarifa nyeti. Kuna tatizo baharini, mpaka sasa samaki kumi na tano aina ya Dragon wamepatikana wakiwa hawana uhai. Japo kwa sasa nimeachana na maswala ya utafiti, yakupasa ufaye jitihada za haraka ili tuweze kujua kuna kiumbe gani baharini mwenye uwezo wa kuwadhuru hawa samaki. Hata kujua ana ukubwa kiasi gani na kama ana madhara kwa binaadamu ili tuweze kuchukua hatua stahiki.” Mr. Faridi akatoa maelezo yake na kumfanya Mtafiti Gibson akune kichwa.
“Hata sisi tumempata mmoja alfajiri hii, bila shaka leo hii nitawasha boti na kuelekea baharini. Kweli kabisa, sitakiwi kulaza damu kwenye hili.” Mtafiti Gibson akaongea na kushikana mikono na mtumishi huyo wa serikali aliyenyanyuka tayari kwa kuondoka.
“Nategemea majibu mazuri kutka kwenye utafiti wako Mr. Gibson.” Mr Faridi akaongea maneno hayo na kuondoka.
Mtafiti Gibson akarudi kwenye meza ya uchunguzi.
“Naenda kwenye maji leo hii, usimpe taarifa hizi mke wangu hata kama akihitaji kujua ni wapi niendapo.” Mr. Gibson akaongea na kumfanya Samira ashangae. Maana mara zote hua wanaenda kufanya tafiti mbalimbali majini wakiwa wote watatu.
“Usiniambie unataka kwenda kufanya utafiti huu peke yako?” Samira akaongea.
“Bila shaka kwenye maji kuna vita. Haihitaji Mtafiti tu wa kawaida kwenda kumchunguza kiumbe aliyeyafanya haya, hivyo sihitaji watu wengine mpate matatizo.” Mr. Gibson akaongea hayo na kumkazia macho Samira.
“Na mimi naenda!”
Ilisikika sauti ya binti alliyeingia ghafla na kumfanya Gibson ashike kichwa. Akamfuata msichana huyo na kumkumbatia.
“Daring, unahitajika kubaki hapa na Samira, acha mimi niende. Nahisi kuna kiumbe wa ajabu na si samaki kama serikali inavyozania.” Mr Gibson akaongea kwa kunong’oneza ili Samira asisikie.
“Nadhani unatambua uwezo wangu. Hapa wakubaki ni Samira, maana ndo hana uwezo wa kupambana.” Mke wa Mtafiti Gibson akashikilia uamuzi wake wa kuongozana na mume wake baharini.
“Naelewa mke wangu, ila ungenipa nafasi ya kunisikiliza ingekua vyema sana. Nahisi hiko kiumbe kinaweza kuwa hatari zaidi ya papa.” Mr. Gibson akaongea huku akionekana kumuonea huruma mke wake.
“Ni mwanamke gani mwenye upendo wa dhati, ambaye anajua mume wake anaenda kwenye hatari na akamuachia? Kunizuia mimi nisiende, ni wazi unahitaji hiyo safari ife. Chagua moja, usiende kwenye maji au twende wote!” Mke wa Mr. Gibson akaongea huku akilegeza macho yake baada ya kukutanisha na mume wake.
“Kwa umuhimu wa hizi tafiti, siwezi kughairi mke wangu.”
“Basi jibu jepesi, tunaenda wote.”
Mke wa Mtafiti akaongea hayo na kumfanya Mr. Gibson kukosa pakutokea.
Wakarudi kwenye meza ya utafiti na kumuachia Samira majukumu ya Maabara hayo na wao wakaanza safari.
Safari ambayo imeleta madhara makubwa. Mr Gibson akasaidiwa akiwa taabani huku mke wake kipenzi akipotelea majini.
Kipi kitaendelea kwenye kisa hiki cha kusisimua?
TYPHIN, Hadithi ya kale, inayoishi.
https://www.youtube.com/watch?v=HWk1-Bltj4U









0 comments:
Post a Comment
comment