‘Hadithi ya kale, inayoishi’
HUSSEIN O. MOLITO
0718 97 56 59/ 0765 68 4870
Mwili mzima ulimtetema, hata yale madaha yake ya utembeaji yakapotea. Nusura taulo limdondoke na kumpa burudani ya macho mlinzi aliyekua akimshuhudia akiwa anatembea kama anasukumwa. Hakika tukio la kufuatwa na polisi mpaka nyumbani lilikua geni kwake. Aliwazoea wale wa usalama barabarani,ila sio hao waliokua na bunduki mikononi.
Baada ya kulifikia kabati lake, hakutaka kuchagua nguo tena, alivuta suruali na kuvaa fulana iliyokua mbele yake. Hakujali kama ilikua imejikunja sana, alichukua Kimomo na kuvaa juu yake. Akajitanda ushungi kisha kutoka mpaka sebuleni. Akakumbuka kua aliacha kitu muhimu sana chumbani, Simu. Aliirejea na kuamua kumpigia simu mama yake.
Simu iliita mara kadhaa bila kupokelewa, aliingiwa na hofu baada ya kuhisi huenda alikua akitumia muda mrefu na kuwakasirisha wale askari wenye ghadhabu.
“Mama pokea!”
Akajisema huku akipiga miguu yake kwenye Marumaru. Simu ikaita mpaka ikakata, lakini mama yake hakupokea.
Akaamua kumpigia baba ake, simu ikaita mara moja tu, kisha mara ya pili ikapokelewa. Sauti ikiwa nzito, Iliashiria kuelemewa na usingizi.
“Asalaam alekum.” Akakumbuka kusalimia baada tu ya simu kupokelewa.
“Aleykum salaam, mbona simu muda huu? Kwema?” Baba yake akauliza maswali mfululizo. Maana si kawaida ya binti yao kuwapigia simu nyakati hizo. Hasa ukilinganisha na siku yenyewe, mwisho wa waki.
“Hakuna usalama baba.”
Sauti ya Samira iliweza kusadifu kile alichozungumza. Mshtuko wa baba baada ya kuambiwa kuwa hakuna usalama, uliweza kumshtua mama yake aliyekua amelala fofofo, huku mkono pekee uliokua unashirikiana na mume wake baada ya kumuwekea kifuani, ukiwa umetolewa kwa nguvu na kuwa sababu ya kuamka kwake.
“Umevamiwa na majambazi?” Baba akauliza kwa hamaki.
“Hapana baba, Askari wapo nje, wamesema wananihitaji kituoni.” Samira akaelezea kinachomtia wasiwasi.
“Umefanya kosa gani binti yangu?” Baba akauliza huku akimfanya mke wake atamani kujua alikua anaongea na mtoto wao yupi. Maana walikua na mabinti wawili waliokua wakiishi mbali nao.
“Nani aliyekupigia simu, Samira au Rabia?” Mama akahamaki.
“Subiri mke wangu nimsikilize kwanza mtoto, kisha nitakushirikisha.”
Baba akaelezea, lakini maneno hayo hayakutosha kumtuliza Bi Mariam. Akamnyang’anya simu mume wake na kuuliza swali bila kujua ni mtoto yupi aliyekua anayeongea naye.
“Yamekufika madhila yapi binti yangu jamani?”
“Askari wamenifuata mpaka nyumbani, sijafanya kosa lolote miye. Ila wamesema niende kituoni.” Samira akaelezea na kumfanya mama yake amtambue kwa sauti.
“Mpigie simu Samira na umuelekeze kituo unachopelekwa. Siye tunajiandaa, tunakuja sasa hivi. Ila usiwe mbishi tu kwa askari, watakuumiza bure kwa mabavu yao.” mama akatoa angalizo na Samira akakata simu. Ndipo alipoamua kumpigia dada yake.
“Dada nimekamatwa na polisi, hivyo nikifika kituoni nitakujulisha nimepekwa kituo gani. Jiandae kabisa.” Samira akatoa taarifa kwa dada yake baada ya kupokea simu. Hakumpa nafasi ya kuhoji, akakata simu na kutoka nje.
Akafunga mlango wake na kwenda kwenye gari ndogo ya askari Bila shuruti.
********
Madaktari waliokua kwenye chumba cha upasuaji, waliendelea kumshona Mtafiti Gibson baada ya kumpiga nusu kaputi.
“Kwa uzoefu wako Dokta Miley, huyu Mtafiti atakua amekumbwa na dhoruba gani?” Daktari mmoja akauliza wakati wakiendelea kukabiliana na majeraha makubwa ya mgonjwa.
“Ni ajabu sana kutokea, hizi ni alama za kucha mfano wa kucha za simba. Sasa baharini hakuna Samaki Mwenye kucha za aina hii. Bila shaka amekumbana na kitu tofauti sana ambacho ni yeye pekee ndoa anakijua.” Daktari akajibu na kuwafanya dakatri wenzake waangaliane.
“Au ameshambuliwa na nguva?” Daktari mmoja akaropoka na kuwafanya wenzake wacheke.
“Hebu Kelvin kuwa serious kidogo ninapouliza maswala ya msingi.” Daktari wa awali akaongea baada ya kicheko kupita.
“Kwani hadithi za nguva bado zipo mpaka sasa?” Dokta Miley akauliza.
“Ni haithi ya kale, ila wapo waliosema viumbe hao walishawahi kuishi miaka dahri iliyopita.” Dokta Kelvin akatetea hoja yake.
“Ndo wapo vile kama tunavyoona kwenye michoro, juu wanawake chini samaki?” Dokta Miley akauliza na kuonekana kuvutiwa na habari hizo za nguva.
“Mimi ninachoamini wapo jinsia zote mbili. Ila wachoraji wanapenda kuwachora wanawake ndo maana huakisi mfano wao. Pia sidhani kama ni warembo kama wanavochorwa pia.” Dokta Kelvin akajitahidi kudadavua.
“Tuendeleeni na kazi, ila sidhani kama viumbe hao walishawahi kuwepo. Ni hadithi kama hadithi zingine za kutunga. Ila itabidi na sisi tukafanye uchunguzi wa kina juu ya huyo kiumbe hatari wa baharini. Maana wananchi wakijua wataingiwa woga hata wa kwenda kuvua samaki.” Dokta Miley akaongea na wenzake wakabaki wanamuangalia.
Juhudi za kuokoa maisha ya mtafiti huyo zikaendelea, mashine zilizokua zinaleta tafsiri ya uhai wa mtu huyo ziliendelea kuwapa faraja.
Baada ya shughuli hiyo iliyochukua takaribani masaa manne, walimaliza salama na kutoka nje ya chumba hicho.
“Dokta Miley, kama unaondoka muda huu. Naomba unipe lift kaka. Leo gari yangu imesumbua. hivyo nimeiacha.”Dokta Kelvin aliongea hayo baada ya kumuwahi Dokta Miley alipokua anatoka nje ya jengo hilo.
“Naelekea Maabara, nahitaji kuchunguza kile kimiminika kilikua kinahusiana na nini… maana inaonekana ni tafiti muhimu sana.” Dokta Miley akaongea na kumfanya mwenzake ashangae.
“Lakini Dokta, tumeambiwa tumtunzie hadi pale atakapoamka. Maana ni yeye ndo anajua umuhimu wa hizi tafiti.” Dokta Kelvin akaongea, na kumfanya Dokta Miley ameangalie kwa ghadhabu.
“Asipoamka? Ukumbuke tukio lililompata si lakawaida. Yatupasa tufanye uchunguzi wa haraka ili tujue chanzo cha ajali yake. Na kama kuna viumbe wa ajabu, basi watu wakatazwe kutumia bahari mpaka pale ufumbuzi utakapopatikana.” Dokta Miley akaongea hayo na kuondoka. Akamuacha mwenzake akiwa anamshangaa tu.
Nusu saa baadae baada ya Rabia kupigiwa simu, akafika kituoni ili kusikiliza kesi inayomkabili mdogo wake.
“Kwa sasa yupo chumba cha mahojiano. We kamsubiri nje.” Rabia alipewa maelekezo hayo na kuamua kutii.
Huko ndani, Samira alikua kwenye chumba cha mahojiano. Askari mmoja aliyevaa mavazi ya kiraia, akafika na kukaa kwenye kiti cha mbele yake.
“Habari binti.”
“salama tu, Shikamoo.” Samira alisalimia huku akitweta.
“Punguza Presha binti, huna kosa lolote, ila kuna vitu muhimu tunahitaji kujua kutoka kwako ili utusaidie kwenye upelelezi wetu. Kuwa na amani.” Askari huyo aliyekua akitumia lugha laini, kidogo aliweza kushawishi fikra za Samira kuamini kuwa anaweza kuwa huru hivi karibuni.
“Naitwa Inspekta Salim, sijui mwenzangu unaitwa nani?” askari huyo akajitambulisha na kuwasha peni yake ambayo ilikua na uwezo wa kurekodi.
“Naitwa Samira, Samira Mohammed.” utambulisho wa binti huyo, ulidhihirisha hofu aliyonayo.
“Samira, mbona najitahidi kukufanya usiniogope ili tuweze kulifanya hili jambo kirafiki? Au kuna kitu kinakutisha humu ndani tukipunguze?” Inspekta akauliza.
Samira akakanusha kwa kutikisa kichwa. Inspekta akachukua simu yake na kumuonesha Samira picha fulani, Akashtuka.
“kwa mshtuko wako, bila shaka unamfahamu. Niambie yupo wapi kwa sasa?” Inspekta akauliza na kurudi kwene kiti chake. Samira akaichukua simu hiyo na kuendelea kuitazama picha ya mtu anayetafutwa.
“Mimi… Mimi nilikua naye jana tu. Hata jina lake silijui.” Samira akaongea na kumrudishia Inspekta Salim simu yake.
“Inasemekana jana mlikua wote siku nzima. Mkaenda mpaka kwenye maduka ya nguo, inakuwaje useme hufahamiani naye? Binti, kuficha kwako muhalifu, kutakufanya uanze kupazoea humu ndani, maana hutorudi nyumbani kama hutosema ukweli.” Inspektaa Salim akaongea na kukaza sauti kidogo.
“Labda nikuelezee tu ilivyokua, nitasema kila kitu ninachokijua kuhusu mtu huyo.” Samira aliongea huku hofu iliyoanza kupotea, ikianza kupanda tena kwa mara nyingine.
“Nipo hapa kuku sikiliza, niambie ilikuaje..” Inspekta Salim akaongea, safari hii akakunja sura, alimaanisha muda wake wa kuwa kazini umefika.
Samira akameza fundo la mate ili aanze kuelezea mkasa mzima.
Huyo mtu ni nani? Ana kesi gani? Je maelezo ya Samira yanaweza kumtoa kwenye hatia, au ni janja tu ya Inspekta Salim? Vipi kuhusu Daktari Miley kuchukua maamuzi mkononi kutafiti kimiminika cha Mtafiti Gibson bila ridhaa yake?
Tukutane siku ya JUMAPILI katika kisa hiki cha kusisimua.
Kumbuka, Riwaya hii inapatikana katika mfumo wa sauti pia. Nenda Youtube kisha search MOLITO BRAND, Au bonyeza link ya Blue, itakupeleka moja kwa moja Youtube kwenye sehemu ya kwanza ya Simulizi hii
https://www.youtube.com/watch?v=HWk1-Bltj4U









0 comments:
Post a Comment
comment